MASWALI NA MAJIBU:
1. Nini maana ya kuasili mtoto kiroho?
Kuasili mtoto kiroho ni sala kwa ajili ya mtoto aliye katika hatari ya kuuawa tumboni mwa mama yake. Sala hii husaliwa kwa miezi tisa na hufanywa kwa kusali fungu moja la rozari kila siku (Mafungu ya Furaha, Mwanga, Uchungu au Utukufu) yaani Baba yetu x1 na Salamu Maria x10, ikifuatiwa na Sala ya kila Siku maalumu ya kumuombea mtoto pamoja na wazazi wake. Sala hii yaweza kufuatiwa na mazoezi mengine ya kiroho.
2. Mazoezi ya kiroho ni nini?
Mazoezi ya kiroho ni kama kuungama mara moja kwa mwezi mmoja, kupokea Ekaristi Takatifu, kuabudu Sakramenti Takatifu, kusoma Neno la Mungu, kufunga, kuvishinda vishawishi na kuwasaidia wahitaji. Sala nyingine kama Litania na Novena zaweza kutumika pia.
3. Je, kuasili mtoto kiroho kwawezekana bila mazoezi ya kiroho?
Ndiyo. Mazoezi ya kiroho ni ya hiari na siyo amri.
4. Kuasili mtoto kiroho kulianzaje?
Jambo hili lilizaliwa baada ya matokeo ya Bikira Maria huko Fatima, katika kuitikia wito wa Mama Bikira Maria Mama wa Mungu kusali Rozari, kufanya toba ya kweli na malipizi ya dhambi zinazoutesa moyo wake Imakulata. Mwaka 1987 zoezi hili lilipelekwa Poland. Kwa mara ya kwanza kituo cha kuasili watoto kiroho kilijengwa huko Warsaw kwenye kanisa la mapadri wa Shirika la Mt. Paulo. Kisha zoezi hili lilienea kila mahali katika nchi ya Poland na katika mataifa mengine.
5. Ni nini matunda ya kuasili mtoto kiroho?
Kuasili mtoto hutibu majeraha ya ndani kabisa yaliyosababishwa na dhambi ya utoaji mimba. Inawasaidia wamama kuhuisha imani yao kwa huruma ya Mungu na kuleta amani katika mioyo yao. Kwa mazoezi haya ya kiroho (kusali, sadaka na kufunga) hasa kwa vijana huwasaidia kuunda tabia zao na kushinda ubinafsi, kugundua furaha ya kuwa mzazi na kuuhuisha upendo kati ya wanandoa kuongozwa na upendo wa Mungu. Kuasili mtoto kiroho huhuisha maana ya mazoezi ya kiroho yaliyoachwa kwa muda mrefu, hii yaweza kuwa sababu kubwa ya kuhuisha moyo wa sala na upendo katika familia.
6. Nani anaweza kuasili mtoto kiroho?
Kila mtu (mlei au mtawa) anaweza kuasili mtoto. Watoto wanaoasili watoto wenzao kiroho wanapaswa kufanya zoezi hili chini ya uangalizi wa wazazi wao.
7. Je, mtu aweza kuasili mtoto mara ngapi?
Mtu aweza kuasili mtoto mara nyingi kwa kuhakikisha anaweza kutekeleza wajibu wake.
8. Je, waweza kuasili mtoto zaidi ya mmoja?
Kuasili mtoto kiroho ni zoezi la mtoto mmoja tu.
9. Je, ni lazima kurudia nadhiri kila wakati?
Ndiyo. Kila mara ukitaka kuanza kuasili mtoto tena unaweka ahadi.
10. Je, tunajua utaifa wa mtoto tunayemuasili?
Hapana, ni Mungu pekee ajuaye mtoto anayeasiliwa.
11. Je, nini kitanipa uhakika kuwa Mungu anasikiliza sala zangu?
Tumaini letu ni kwa Mungu anayeweza yote kwa huruma yake isiyo na mipaka. Mungu ni mpaji wa uhai na mpango wake ni kuwa kila mtoto aliyetungwa mimba aishi na kuzungukwa na upendo wa wazazi wake.
12. Je, nikisahau kusali kwa siku chache sali hii imesitishwa?
Hapana, kwa sababu kusahau siyo kwa makusudi. Fidia siku ulizoacha kusali.
13. Je, nikiacha sala hii kwa makusudi itakuwaje?
Katika hali hii ongeza ari ya kusali na kusoma Neno la Mungu, kufunga kwa hiari bila shuruti.
14. Je, watu wasioishi maisha ya sakramenti waweza kuasili mtoto kiroho?
Ndiyo, wanaweza.
15. Je, wagonjwa, watu wasiojiweza na wazee waweza kuasili mtoto kiroho?
Ndiyo, watu hawa wanaweza kuasili mtoto kiroho.
16. Je, ni lazima kuweka kiapo cha kuasili mtoto kiroho katika Kanisa na mbele ya padre?
Hapana. Sio lazima kweka kiapo mbele ya padre. Unaweza kuweka kiapo hiki kibinafsi.
17. Je, inaruhusiwa kuasili mtoto kiroho kwa njia ya redio?
Ndiyo. Kwa njia ya kusikiliza sala, kwa ahadi ya kuasili maisha ya mtoto (iliyoandikwa hapo juu) na tafadhali umpe taarifa kwa padri au tuma taarifa barua pepe ku*********************@gm***.com
18. Je, wawezaje, kuweka ahadi ya kuasili mtoto kiroho binafsi?
Sali sala ya kuweka ahadi (ni vizuri isaliwe mbele ya msalaba au sanamu takatifu) na tangu hapo kwa miezi tisa sali mojawapo ya fungu la rozari na usali kwa nia ya mtoto na wazazi wake. Ni vizuri kuandika tarehe ya kuanza na kumaliza ili kukumbuka. (ni wiki arobaini. kwa mfano ukianza tarehe 25 mwezi wa tatu utasali hadi mwezi wa kumi na mbili tarehe 25)
19 . Namna gani ya kueneza sala ya kuasili mtoto kiroho?
Tafuta watu wanaopenda kuasili watoto kiroho. Pata ruhusa toka kwa paroko kuwaelekeza watu wanaopenda kuasili watoto kiroho kuweka ahadi za kuasili watoto kanisani au kama ilivyoandikwa hapo juu.