Somo wa zoezi la Kuasili Kiroho

Mtakatifu Papa Yohane Paulo II 

Baba Mtakatifu (Karol Józef Wojtyła) alizaliwa tarehe 18/5/1920 mjini Wadowice, kusini mwa nchi ya Poland, akiwa mtoto wa tatu na wa mwisho kwa wazazi wake Karol Wojtyła na Emilia Kaczorowska. Dada yake Olga alikufa kabla Karol hajazaliwa; hivyo, alihusiana sana na kaka yake Edmund, mpaka huyo alipokufa kwa tetekuanga kutokana na kazi yake ya udaktari.
Akiwa kijana, Karol alipenda sana spoti akacheza mara nyingi kandanda kama kipa. Miaka ya malezi yake iliathiriwa na uhusiano mkubwa na Wayahudi wengi wa Wadowice. Mara nyingi kulikuwa na mechi kati ya Wakatoliki na Wayahudi, naye alijitolea kuwa kipa wa Wayahudi timu yao ilipopungukiwa wachezaji.
Katikati ya mwaka 1938, Karol na baba yake walihamia Kraków, alipojiunga na chuo kikuu maarufu cha “Jagiellonian University”. Huko akisoma filolojia na lugha 12 tofauti, alijitolea kusaidia kama mkutubi. Alipolazimishwa kujiunga na jeshi [36th Infantry Regiment (Poland) Academic Legion], alikataa kufyatua risasi. Pia aliigiza na kutunga mwenyewe tamthilia.
Mwaka 1939 Ujerumani wa Hitler ulivamia Polandi ukafunga chuo kikuu hicho, huku wanaume wote wakidaiwa kufanya kazi. Hivyo, tangu mwaka 1940 hadi 1944, Karol alifanya kazi mbalimbali za mikono asije akahamishiwa katika makambi ya KZ.
Baba yake alifariki kwa mpasuko wa moyo mwaka 1941, akimuacha peke yake. Miaka 40 baadaye alisema,“Sikuwepo mama alipofariki, sikuwepo kaka alipofariki, sikuwepo baba alipofariki. Kufikia umri wa miaka 20 nilikuwa nimeshapoteza wapenzi wangu wote”.

Ndipo alipoanza kufikiria sana wito wa upadre, ambao polepole ukawa ‘jambo la ndani lenye hakika ya hali ya juu’. Kwa sababu hiyo , mnamo Oktoba 1942, alipopiga hodi kwenye nyumba ya Askofu Mkuu wa Kraków, Kardinali Adam Stefan Sapieha, akaomba asomee upadre. Mapema akawa anasoma kwa siri katika seminari iliyoendeshwa huko kwa maficho.

 

Tarehe 29 Februari 1944, Karol aligongwa na lori la Kijerumani. Tofauti na kawaida, alipelekwa hospitalini alipotibiwa wiki mbili. Kunusurika ajali hiyo kulimthibitisha katika wito wake. Tarehe 6 Agosti 1944, ‘Black Sunday’, askari wa Gestapo walijaribu kukamata wavulana wote wa Kraków wasije wakaanza mapambano dhidi yao kama ilivyotokea Warsaw. Karol alifaulu kujificha katika handaki la nyumba iliyokaguliwa na askari, wakati vijana zaidi ya elfu nane walikamatwa siku hiyo. Halafu aakapata hifadhi nyumbani kwa Askofu Mkuu hadi Wajerumani walipofukuzwa tarehe 17 Januari 1945.
Mwezi huohuo, alimuokoa Edith Zierer, binti Myahudi wa miaka 14 ambaye alikuwa amekimbia kambi la Częstochowa lakini akazimia kwenye reli. Karol akampandisha juu ya treni na kumfikisha salama mjini Kraków. B’nai B’rith na makundi mengine ya Kiyahudi yamethibitisha kuwa Karol aliokoa wengine vilevile dhidi ya dhuluma ya Wanazi.
Kisha kumaliza masomo yake seminarini, tarehe 1 Novemba 1946 Karol alipadrishwa na kardinali Adam Stefan Sapieha.
Baada ya hapo alitumwa Roma akasome teolojia kwenye chuo kikuu cha Kipapa Angelicum, alipojipatia digrii ya pili na ya tatu katika teolojia. Udaktari huo, ambao ulifuatwa na mwingine, ulipatikana kwa kuchambua Fundisho la Imani kadiri ya Mt. Yohane wa Msalaba.
Akirudi Polandi katikati ya mwaka 1948 alipangiwa kazi yake ya kichungaji ya kwanza katika kijiji cha Niegowić, kilometa 25 kutoka Kraków. Alipofika huko tu, alipiga magoti na kubusu ardhi kama atakapofanya mara nyingi katika safari zake za kimataifa akifika kwenye nchi fulani. Tendo hilo liliiga lile la Mtakatifu Yohane Maria Vianney.
Mnamo Machi 1949 alihamishiwa parokia ya Mtakatifu Florian mjini Kraków, akaanza kufundisha maadili katika Jagiellonian University halafu katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Lublin. Wakati huo alikusanya vijana 20 hivi walioanza kujiita Rodzinka, “familia ndogo”. Walikuwa wakikutana kwa kusali, kujadili falsafa, na kusaidia vipofu na wagonjwa. Polepole kundi hilo lilifikia washiriki 200 hivi, nao wakajiongezea fani za michezo na spoti.
Mwaka 1954 alipata udaktari wa pili katika falsafa, kwa kutathmini uwezekano wa kufundisha maadili ya Kikatoliki kwa kutumia fenomenolojia ya Max Scheller. Lakini serikali ya Kikomunisti ilimzuia asipewe digri hiyo mpaka mwaka 1957.
Wakati huo, Padre Wojtyła aliandika mfululizo wa makala kuhusu mada za Kikanisa katika gazeti la kila wiki la jimbo Tygodnik Powszechny.
Katika miaka 12 ya kwanza ya upadre wake alitunga pia fasihi mpya mbalimbali kuhusu vita, hali ya maisha chini ya Ukomunisti, majukumu ya kichungaji n.k. Lakini alichapisha maandishi hayo kwa kutumia jina la bandia Andrzej Jawień au Stanisław Andrzej Gruda – tofauti na maandishi yake ya kidini yaliyotolewa kwa jina lake halisi.
Mwaka 1960, Wojtyła alitoa kitabu muhimu cha maadilidini ‘Upendo na Uwajibikaji’, akitetea mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu ndoa kwa kutumia mtazamo wa kifalsafa.
Tarehe 4 Julai 1958 Papa Pio X alimteua Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Kraków. Aliitwa Warsaw akutane na Mkuu wa Maaskofu wa Polandi, kardinali Stefan Wyszyński, aliyemuarifu kuhusu uteuzi huo. Kisha kukubali kuwa Askofu Msaidizi wa askofu mkuu Eugeniusz Baziak, aliwekwa wakfu (akipewa jimbo la zamani la Ombi) tarehe 28 Septemba 1958. Akiwa na miaka 38 tu, alikuwa kijana kuliko maaskofu wote wa Polandi wakati ule. Baada ya kifo cha Askofu Mkuu Eugeniusz Baziak mnamo Juni 1962, tarehe 16 Julai, Karol Wojtyła alichaguliwa asimamie jimbo kama Vicar Capitular. Tarehe 13 Januari 1964, Papa Paulo VI alimteua kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kraków.
Baba Askofu Karol Wojtyła alishiriki toka mwanzo hadi mwisho Mtaguso wa pili wa Vatikan (1962–1965), akichangia hasa hati ya Dignitatis Humanae na Gaudium et Spes.
Tarehe 26 Juni 1967, Paulo VI alimteua kardinali akapewa kanisa la San Cesareo in Palatio.
Mwaka 1967 alichangia pia hati Humanae Vitae iliyokataza tena utoaji mimba na teknolojia ya uzazi wa mpango.
Mnamo Agosti 1978, Mwadhama Kardinali Karol Wojtyła alishiriki uchaguzi wa Papa Yohane Paulo I, aliyefariki baada ya siku 33 tu.
Uchaguzi wa pili wa mwaka huo 1978 ulianza tarehe 14 Oktoba na Wojtyła akachaguliwa walipopiga kura mara ya nane. Hapo alijichagulia jina la Yohane Paulo II kwa heshima ya watangulizi wake wa mwisho.
Akiwa na miaka 58 tu, alikuwa kijana kuliko Mapapa wote waliochaguliwa baada ya Papa Pius IX mwaka 1846, aliyekuwa na miaka 54. Ibada ya kuanzia rasmi Upapa wake ilifanyika tarehe 22 Oktoba 1978.
Mwaka 1981 alitoa barua yake maalum kwa Kanisa zima ambayo inaitwa encyclical letter – yenye kichwa cha habari: “DIVES IN MISERICORDIA” (Tajiri wa Huruma), ambamo alimtaja Kristo kuwa “Umwilisho wa Huruma” na “chemchemi isiyokauka ya neema” (8). Anaendelea kusisitiza kuwa “mpango wa Kristo wa kimasiha, mpango wa Huruma” hauna budi kuwa “mpango wa watu wake, yaani Kanisa lake” (8).
Katika barua hiyo, Baba Mtakatifu anaeleza kwa kirefu kuwa Kanisa – hasa katika nyakati zetu hizi mpya – lina HAKI NA WAJIBU wa kukiri na kutangaza Huruma ya Mungu, kuieneza katika mazingira na maisha ya watu na kuomba Huruma ya Mungu kwa ajili ya ulimwengu mzima (12-15).
Mwaka mmoja baada ya kutoa TAJIRI WA HURUMA Baba Mtakatifu alitembelea mahali pa hija katika mji wa Collevalenza, Italia, paitwapo UPENDO WENYE HURUMA, katika safari yake ya kwanza nje ya Roma baada ya jaribio la kumuua (lililotokea 13/5/1981). Akiwa huko alisisitiza juu ya Ujumbe wa Huruma na akaeleza kuwa toka mwanzoni kabisa mwa utume wake kama Papa, ameona kuwa Ujumbe huu ni KAZI YAKE MAALUM, aliyopewa na Mungu “katika hali ya sasa ya mwanadamu, Kanisa na dunia hii”.
Mnamo tarehe 1 hadi 5 mwezi wa tisa mwaka wa 1990 Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alifanya ziara ya kichungaji nchini Tanzania.
Tarehe 10 Aprili 1991, akiongea hadharani, Baba Mtakatifu aliongea juu ya Sista Faustina, akionyesha jinsi anavyomheshimu sana na kumhusisha na barua yake pamoja na kusisitizia jukumu lake Faustina katika kuleta ujumbe huu kwa dunia nzima: “Maneno ya barua yangu kuhusu Huruma ya Mungu (TAJIRI WA HURUMA) yanatuhusu sisi kwa namna ya pekee… Yanatukumbusha picha ya Mtumishi wa Mungu, Sista Faustina Kowalska. Huyu mtawa wa kike ameleta Ujumbe wa Pasaka kuhusu Yesu Mwenye Huruma karibu zaidi kwa Poland na ulimwengu mzima”.
Baada ya kuugua miaka kadhaa ugonjwa wa Parkinson bila ya kuacha utume wake, mwaka 2005 alilazwa mara kadhaa katika Agostino Gemelli University Polyclinic ambapo hatimaye alifariki tarehe 2 Aprili. Maneno yake ya mwisho yalikuwa – “Acheni niende nyumbani mwa Baba”. Siku hiyo ilikuwa ni Jumamosi kabla ya Sherehe ya Huruma ya Mungu.
Misa ya mazishi yake tarehe 8 Aprili ilivunja rekodi ya washiriki na ya viongozi wa nchi waliohudhuria.
Papa Benedikto XVI aliruhusu mchakato wa kumtangaza mtangulizi wake mwenye heri na mtakatifu uwahi kuanza. Baada ya utafiti juu ya ushujaa wa maadili yake, juu ya maandishi yake na juu ya muujiza uliomtokea sista Marie Simon- Pierre wa Ufaransa kwa maombezi ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, ametangazwa na mwandamizi wake Papa Benedikto XVI kuwa Mwenye Heri tarehe 1 Mei 2011, halafu Papa Fransisko akamtangaza Mtakatifu tarehe 27 Aprili 2014 pamoja na Papa Yohane XXIII. Ilikuwa ni Dominika ya Sherehe ya Huruma ya Mungu.
Sikukuu yake huadhimishwa kila mwaka tarehe 22 Oktoba, kulingana na siku ya kuanza rasmi huduma yake ya Kipapa.

Mtakatifu Sista Faustina

Mtakatifu Sista Faustina Kowalska alizaliwa na kupewa jina Helena Kowalska katika kijiji cha Głogowiec magharibi mwa Łódź , Poland, tarehe 25 Agosti 1905. Alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto kumi. Alipokuwa na umri upatao miaka ishirini, alijiunga na Shirika la Masista wa Bibi yetu wa Huruma ambao hujitoa mhanga kuwahudumia, kuwatunza na kuwaelemisha wasichana wenye matatizo, waishio katika mazingira hatarishi na wasiojiweza. Mwaka uliofuata alifunga nadhiri na kupewa jina Sista Maria Faustina naye akaongeza “wa Ekaristi Takatifu” kwa ruhusa maalum kadiri ya desturi ya Shirika lake. Katika miaka ya 1930, Sista Faustina alipokea ujumbe kutoka kwa Bwana Yesu kuhusu “HURUMA YA BWANA” na akaambiwa autangaze na kuueneza duniani kote. Aliombwa kuwa mtume na mwandishi wa Huruma ya Mungu, mfano wa kuonyesha huruma kwa wengine na chombo cha kusisitiza tena na tena juu ya mpango wa Mungu wa Huruma kwa dunia nzima. Haikuwa kazi rahisi. Maisha yake yote kama ya Kristo mwenyewe yalikuwa ya kujitoa sadaka – maisha kwa ajili ya wengine. Kwa ombi tukufu la Bwana wetu, alijitoa kwa hiari yake kuunganisha mateso yake binafsi na yale ya Bwana wetu kwa kulipia dhambi za wengine. Katika maisha yake ya kila siku alionyesha huruma kwa vitendo, ili kuwaletea wengine furaha na amani na kwa kuandika juu ya Huruma ya Mungu angewatia wengine moyo ili wamtumainie Bwana na hivyo waiandae dunia kwa Ujio wake wa pili. Alijiona hastahili hata kidogo na akaogopa sana kuandika lolote lakini ilibidi amtii baba yake wa kiroho pamoja na Yesu mwenyewe aliyemshauri atii agizo la mwungamishi wake. Basi, tangu 1934 alianza kuandika shajara yake (diary). Kwa miaka minne aliandika maono yaliyofunuliwa kwake na Mungu na mafumbo yaliyoambatana nayo ikiwa ni pamoja na tafakari zake, sala, mashairi, tenzi za roho, maoni yake na sala zake mwenyewe. Matokeo yake ni madaftari sita yenye jumla ya kurasa mia sita hivi. Madaftari hayo yaliunganishwa baadaye pamoja na kuchapishwa kama kitabu kimoja cha Shajara ambacho kwa lugha ya kawaida kinarudia na kuweka wazi simulizi la Injili kuhusu Upendo wa Mungu kwa watu wake na kusisitizia hasa umuhimu wa kuamini na kutumainia upendo wake unaojitokeza katika matendo maishani mwetu. Vile vile kinaonyesha wazi mfano usio wa kawaida wa jinsi ya kuitikia Huruma ya Mungu na kuidhihirisha kwa wengine. Msingi wa maisha ya kiroho ya Mt. Sista Faustina ulikuwa ni unyenyekevu mwingi, usafi wa nia na utii wa kimapendo kwa mapenzi ya Mungu, akifuasa na kuiga fadhila za Bikira Maria Mtakatifu. Ibada yake maalum kwa Maria Imakulata na kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho ilimpa nguvu ya kuvumilia maumivu na mateso yake yote kama majitoleo kwa Mungu kwa niaba ya Kanisa na kwa wale wenye shida maalum, hasa wadhambi na wanaokufa. Sista Faustina alijua kwamba Mkristo hawezi kukua na kukomaa katika imani yake na 34 kulelewa katika hadhi ya kuwa Mtume wa Huruma ya Mungu kama hatasimika nafsi yake imara juu ya mawe matatu ya uzima – mafiga matatu – ambayo hayapatikani katika madhehebu mengine (isipokuwa Orthodox Churches) maana yana chapa ya Kanisa Katoliki tu. Nayo ni Upatanisho, Ekaristi Takatifu na Ibada Hai kwa Mama Bikira Maria. Ewe Mkristo, usiposimika chungu cha nafsi yako, utu wako, imani yako, wito wako juu ya mafiga haya matatu, hutaiva na kukomaa. Mkristo anayeishi mbali na mafiga matatu haya ama anatafuta mafiga mbadala – atabaki mbichi milele. Sista Faustina aliandika na kuteseka kwa siri, kwani ni baba yake wa kiroho tu na baadhi ya wakubwa wake walijua yaliyokuwa yanampata. Baada ya kifo chake kwa ugonjwa wa T.B. tarehe 5/10/1938 hata marafiki zake wa karibu walishangaa mno walipogundua maradhi aliyokuwa nayo, ingawa katika uhai wake alikuwa akionekana mwenye furaha na mnyenyekevu daima! Ndani kabisa moyoni mwake alikuwa ameweka agizo la Mungu katika Injili lisemalo “iweni na huruma kama Baba yenu wa mbinguni alivyo na Huruma” pamoja na ushauri wa baba yake wa kiroho (Padre muungamishaji wake) Mwenye Heri Michał Sopoćko kuwa ahakikishe kwamba katika matendo yake kila atakayekutana naye ataondoka kwa furaha. Ujumbe wa Huruma uliopokelewa na Sista Faustina hivi sasa unasambazwa duniani kote; Kanisa limemtambua kama Mwenye Heri na Mtakatifu na Shajara yake – HURUMA YA MUNGU ROHONI MWANGU – imekuwa mwongozo kwa Ujumbe na Ibada kwa Huruma ya Mungu kwa dunia nzima. Si ajabu kwani aliambiwa kuwa Ujumbe huu ungeenea kutokana na maandishi yake kwa faida ya roho za watu. Katika usemi wa kinabii alikuwa ametangaza: “Nina hakika kuwa kifo changu hakitakuwa mwisho wa utume wangu, bali utakuwa ndiyo mwanzo. Enyi roho zenye mashaka, nitawafunika kwa taji za kimbingu ili kuwathibitishia wema wa Mungu” (281).

Mwenyeheri Padre Michał Sopoćko

Mtume Mkuu wa tatu wa Huruma ya Mungu ni Mwenye Heri Padre Michał (Michael) Sopoćko, baba wa kiroho na muungamishaji wa Mt. Sista Faustina. Kwa bahati mbaya, Mtume huyu mwenye mastahili makubwa kabisa katika kazi ya kutunza na kueneza Ujumbe na Ibada ya Huruma ya Mungu hajatambuliwa na kupewa heshima na nafasi sawa na Mt. Sista Faustina na Mt. Yohane Paulo II. Hebu, tumtazame kwa karibu zaidi Padre huyo ambaye Yesu, Mfalme wa Huruma, alimpa kazi maalum katika mpango wake wa kutangaza Huruma yake kwa dunia nzima. Padre Michał Sopoćko alizaliwa 1 Novemba 1888 roku katika kijiji cha Juszewszczyzna (au kwa jina jingine – Nowosady) jirani na mji wa Vilnius (nchi ya Lithuania kwa sasa). Baada ya kuhitimu elimu ya msingi na ya sekondari katika mji wa Oszmian alijiunga na seminari mjini Vilnius mwaka 1910. Akapadrishwa mwaka 1914. Katika miaka ya 1914-1918 alifanya utume katika parokia ya Taboryszki kama paroko msaidizi. Mwaka 1918 alipelekwa Warsaw na kusomea teolojia ya maadili (moral theology) katika Chuo Kikuu cha Warsaw. Alifaulu vizuri katika masomo yake na kutunukiwa kwanza stashahada mwaka 1923 na hatimaye shahada ya uzamili katika teolojia ya maadili mwaka 1926. Sambamba na masomo hayo alisomea pia Chuo Kikuu cha Ualimu mwaka 1922-1924. Aidha, kuanzia mwaka 1919 alifanya utume kama baba wa kiroho katika jeshi la wananchi la Poland (military chaplain). Mwaka 1924 alirejea jimbo lake la nyumbani akiendelea na utume jeshini katika mji wa Vilnius hadi mwaka 1929. Mnamo mwaka 1927 aliteuliwa kuwa baba wa kiroho wa seminari kuu ya Vilnius. Mwaka 1928 aliteuliwa kuwa makamu profesa wa Idara ya Teolojia ya Chuo Kikuu cha Stefan Batory mjini Vilnius na mwalimu katika seminari kuu. Mwaka 1932 alipunguziwa kazi ya baba wa kiroho ili aendelee na masomo na kazi ya profesa katika Chuo Kikuu. Mwaka 1934 alipata digrii katika teolojia ya kichungaji. Akaendelea na ufundishaji katika Chuo Kikuu cha Stefan Batory hadi Chuo kilipofungwa wakati wa vita ya pili ya dunia. Akiwa mlezi na mwalimu katika seminari na chuo kikuu aliandika makala nyingi katika nyanja za teolojia 35 ya kichungaji, mahubiri, katekesi na ualimu. Aidha, aliandika mada mbalimbali zihusuzo mahusiano ya dini na maswla ya jamii. Wakati wa vita ya pili ya dunia alisalimika kukamatwa na Wajerumani na aliendelea kuishi mafichoni kwa muda wa miaka miwili na nusu katika maeneo mbalimbali ya mji wa Vilnius na vitongoji vyake. Mwaka 1944 seminari kuu ilifunguliwa tena na Padre Michał alianza kufundisha tena. Mwaka 1945 seminari ilifungwa na Warusi na kuhamishiwa mjini Białystok. Wakati hu alisaidia katika kazi za kitume kwenye kanisa la Mt. Yohane, Vilnius na kufundisha dini kinyume cha amri za Warusi Wakomunisti. Ilipoonekana kwamba atakamatwa nao, mwaka 1947 Padre koalikimbilia Białystok. Huko alifundisha katika seminari kuu – ualimu, katekesi, mahubiri, teolojia ya kichungaji, teolojia ya maadili. Aidha, akajihusisha na jitihada za kuwasaidia walevi kuacha pombe. Alifundisha pia lugha ya kilatini na kirusi. Miaka ya 1951 hadi 1958 alisimamia mafunzo ya katekesi kwa Watawa na Walei na katika miongo ya 1950 na 1960 alisimamia mafundisho ya teolojia katika parokia ya Białystok. Mwaka 1962 Padre Michał alistaafu lakini akaendelea na utume wake katika kikanisa cha nyumba ya kitawa ya Masista Wamisionari wa Familia Takatifu. Akapanua kikanisa hicho mnamo mwaka wa 1957. Hadi umzi lake la mwish , Padre Michał ko alijituma sana kushiriki kikamilifu katika maisha ya jimbo lake kwa kutumia taaluma yake. Alifariki tarehe 15 Februari 1975 katika nyumba ya Watawa Wamisionari wa Familia Takatifu. Padre Michał Sopoćko alimtumikia Mungu na Kanisa lake kwa nguvu zake zote. Alikuwa na bidii ya ajabu katika maisha yake ya kiroho yenye kina kirefu cha utakatifu. Alijibidisha kutafuta utukufu wa Mungu huku akionyesha wingi wa karama za Roho Mtakatifu alizojaliwa na Mungu akiwa Padre parokiani, mwalimu wa dini, mkufunzi na profesa katika seminari na chuo kikuu, baba wa kiroho seminari na katika jeshi la wananchi, afisa wa ustawi wa jamii, mjenzi wa makanisa. Pamoja na sifa zote hizo kemkem alizokuwa nazo, sifa yake kuu kabisa na ya pekee inatokana na utumishi wake kwa Ujumbe na Ibada ya Huruma ya Mungu. Yeye ndiye aliyeteuliwa na Yesu, Mfalme wa Huruma, kuwa baba wa kiroho na muungamishaji wa Mt. Sista Faustina Kowalska. Yeye ndiye anayestahili kwa haki zote na mastahili yake yote kuitwa Mtume wa Huruma ya Mungu sambamba na Sista Faustina na Papa Yohane Paulo II. Padre Michał akivutiwa sana na maono ya Yesu wa Huruma aliyopewa Mt. Sista Faustina, alijitolea kikamilifu kueneza Ujumbe na Ibada kwa Huruma ya Mungu kwa njia ya uandishi wake, mahubiri, jitihada zake ili Kanisa Takatifu lipate kutambua na kutangaza Sikukuu ya Huruma ya Mungu. Yeye ndiye aliyesaidia kumpata msanii aliyechora picha ya kwanza kabisa ya Yesu, Mfalme wa Huruma. Padre Michał alimsaidia pia Sista Faustina kuanzisha Shirika la Watawa wa Yesu wa Huruma. Kwa kutambua sifa zote hizo za Padre Michał, mwaka 1987 mchakato wa kumtangaza kuwa mwenye heri na hatimaye mtakatifu ulianza rasmi katika Jimbo Kuu la Białystok. Mchakato ulikamilika katika ngazi ya Jimbo mwaka 1993. Mwaka 2002 nyaraka zote pamoja na historia ya maisha ya Padre Sopoćko zikiwa zimeunganishwa katika kitabu kiitwacho ‘Positio’ zilipelekwa Vatikan katika Idara ya Watakatifu. Mwaka 2004 kamati ya wanateolojia ilikubali ‘Positio’ kisha kamati ya Makardinali ilipokea na kuidhinisha tamko la wanateolojia. Tarehe 20/12/2004 mbele ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II hati ya kutambua ushujaa wa fadhila za Mtumishi wa Mungu Padre Michał Sopoćko ilitangazwa. Mwezi wa Desemba 2007 Idara ya Watakatifu ya Vatikano ilitambua na kuthibitisha muujiza uliotokea kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu Padre Michał.

Padre Michał Sopoćko alitangazwa kuwa Mwenye Heri tarehe 28/9/2008 katika Kituo cha Hija cha Huruma ya Mungu mjini Białystok ambamo Masalia yake Matakatifu yanahifadhiwa kwa heshima kubwa.