Ukuwaji wa mtoto tumboni mwa mama

Wiki ya 1

Katika wiki ya kwanza ukuaji wa mwanadamu huanza kwa yai kurutubishwa na mbegu kwa kutengeneza seli ya kwanza. Baada ya mimba kutungwa, seli ya kwanza hugawanyika na kutengeneza seli nyingine nyingi. Kisha kichanga huanza safari toka mirija ya falopia hadi kwenye mji wa uzazi.

 

Wiki ya 2

Wiki ya pili katika maendeleo ya binadamu inahusisha upandikizaji wa kichanga katika mji wa uzazi na ukuaji wa seli ndogo ndogo za mfuko wa uzazi (plasenta)

 

Wiki ya 3

Katika wiki ya tatu kichanga huwa na matabaka matatu ya seli, tabaka la kwanza na la juu linatengeneza ngozi, mfumo wa fahamu na masikio. Tabaka la kati la seli hutengeneza moyo, mfumo wa damu, mifupa, figo na mfumo wa uzazi, tabaka la ndani la seli hutengeneza mapafu na utumbo. Katika hatua hii placenta hukamilika pia.

 

Wiki ya 4

Katika wiki ya nne ya ukuaji wa mtoto tumboni mwa mama yake viungo mbalimbali vya mwili hutengenezwa, kiungo cha kwanza kabisa ambacho hutengenezwa ni moyo, ubongo na mfumo wa fahamu wa mtoto pia huanza kukua taratibu, mifumo ya chakula, uzazi na mzunguko wa damu huanza kutengenezwa pia.

 

Wiki ya 5

Hapa ubongo wa mtoto na uso hukua na kuchukua nafasi yake katika mwili wa mtoto. Pua ya mtoto hutengenezwa katika hatua hii. Mikono na miguu ya mtoto huanza kutengenezwa. Moyo hukua na kugawanyika katika vyumba vinne yaani ventriko 2 na auriko 2.

 

Wiki ya 6

Katika wiki ya sita ya ukuaji wa mtoto miguu hukua vizuri na kuonekana, vidole huanza kutengenezwa, pia masikio ya mtoto hutengenezwa katika hatua hii. Mpaka mwisho wa wiki ya sita mtoto huwa na urefu wa milimita 11 hadi 14.

 

Wiki ya 7

Mikono ya mtoto hukua na viwiko vya mikono huonekana. Vidole vya miguu na kope huonekana. Kichwa cha mtoto huwa kikubwa, hapa bado kidevu hakijawa na muundo unaoonekana. Sehemu ya ubongo inayohusiana na harufu hukamilika na kuonekana. Mpaka mwisho wa wiki ya saba mtoto anakuwa na urefu usiopungua milimita 16 hadi 18 sawa na inchi 3/4

 

Wiki ya 8

Katika wiki ya nane, mtoto anakuwa na kichwa cha mviringo zaidi na anaweza kukunja na kunyoosha viwiko vya mikono yake. Vidole vya mikono na miguu huwa virefu na kuonekana vizuri. Macho na masikio hukamilika na kuonekana. Hapa kitovu huonekana vizuri, moyo unakuwa umekamilika kabisa na pua inajiimarisha katika hisia ya harufu.

 

Wiki ya 9

Katika wiki ya tisa mtoto anaonekana vizuri kabisa. Seli nyekundu za damu na ini huanza kutengenezwa katika hatua hii. Sehemu za siri ambazo huonyesha kama mtoto ni wa kiume au wa kike hukua katika hatua hii. Katika hatua hii mtoto huwa na urefu wa sentimita 5.

 

Wiki ya 10

Katika wiki ya kumi kucha za vidole vya mikononi hukua, uso wa mtoto huonekana vizuri zaidi, utumbo unakua na kufungiwa ndani ya tumbo. Kuanzia sasa mifupa laini huwa migumu kuanzia na fuvu alafu mifupa mingine mwilini, hapa mtoto huwa na uzito wa 14g.

 

Wiki ya 11

Hapa mtoto huanza kutengeneza taka mwili kama mkojo. Ngozi ya mtoto ni laini sana na taratibu inaanza kuwa ngumu na nzito. Via vya uzazi huanza kutengenezwa. Hapa pia mtoto ameshaweza kunyonya kidole gumba chake.

 

Wiki ya 12

Shingo ya mtoto imetengenezwa vizuri na miguu yake imeshakamilika. Seli nyekundu za damu zinaendelea kuimarika. Hapa jinsia ya mtoto yaweza kuonekana kupitia kipimo cha ultrasound. Nywele laini huanza kuota kichwani na mwilini kwa mtoto. Mtoto huchezesha mikono, miguu na macho yake kwa namna nzuri zaidi.

 

Wiki ya 13

Mtoto ana kipimo cha karibu sentimita 10.1 kutoka kichwani hadi chini akiwa na uzito wa gram 70. Inakadiriwa mtoto kuwa na ukubwa sawa na tufaha. Mifumo ya kupumua ya mtoto na ya uyeyushaji wa chakula unaboreka zaidi. Anatumia uwezo wake wa kumeza na kunyonya kupumua maji ya amniotic, ambayo ni mazoezi mazuri kwa mapafu yake yanayokua. Wakati huu mifupa yake ni migumu na tishu za misuli zinaendelea kukua.

 

Wiki ya 14

Misuli ya shingo na mgongo huimarika zaidi na kichwa huweza kukaa wima. Hapa mtoto ana uwezo wa kukutanisha mikono yake pamoja.

 

Wiki ya 15

Kucha za vidole vya miguu hukua mtoto anakuwa mchangamfu katika tumbo, huweza kugeuka na kucheza cheza ndani ya tumbo. Moyo wake huweza kusukuma angalau matone 100 ya damu kila siku. Alama za vidole na nyayo huanza kuweka utofauti na upekee wake.

 

Wiki ya 16

Mtoto huwa na urefu wa sentimita 14.2 na uzito wa 190g. Masikio ya mtoto huanza kuonekana vizuri na anaweza kusikia. Macho huanza kuona na mfumo wa chakula huanza kufanya kazi.

 

Wiki ya 17

Mikono na miguu ya mtoto inakuwa kwenye uwiano sawa na sehemu nyingine za mwili wa mtoto. Nywele laini huanza kuota kichwani. Ubongo wa mtoto hutengeneza sehemu mbalimbali zinazohusika na harufu, ladha, kuona, kusikia na kugusa. Mafuta laini huanza kuifunika ngozi ya mtoto ili kuilinda na michubuko.

 

Wiki ya 18

Katika wiki ya 18 ya mimba mama anaweza kuhisi mtoto anavyosogea tumboni mwake. Mtoto hulala na kuamka mara nyingi. Mtoto huamshwa na kelele au mtikisiko toka kwa mama yake. Kipindi hiki mtoto huwa na urefu wa ndizi na uzito wa 300g.

 

Wiki ya 19

Mtoto anakuwa na vinyweleo mwili mzima ili kushikilia mafuta mazito yanayoifunika ngozi, uwezo wa kunyonya wa mtoto hukua kwa kunyonya kidole gumba. Ngozi ya mtoto huanza kukomaaa na kutengeneza mishipa ya damu chini yake, mtoto anaweza kufungua mdomo, kupiga miayo na kunyonya.

 

Wiki ya 20

Macho ya mtoto na nywele huonekana. Mafuta mazito humzunguka mtoto kwa ajili ya kuleta joto. Kwa watoto wa kiume via vya uzazi huanza kuonekana. Mtoto anaendelea kunyonya maji yaliyopo ndani ya plasenta ambayo ni mazoezi mazuri kwa ajili ya kunyonya baada ya kuzaliwa.

 

Wiki ya 21

Hapa mtoto anakuwa na uzito wa 500g na urefu wa sentimita 29. Mtoto huweza kupepesa macho kwa haraka haraka. Mtoto anahisi sauti yeyote.

 

Wiki ya 22

Hapa kope hucheza na macho hufunguka, mfumo wa kulala na kuamka huonekana vizuri zaidi. Ubongo wa mtoto hukua vizuri zaidi. Misuli ya uso huimarika na mtoto huonyesha ishara mbalimbali kama kutabasamu.

 

Wiki ya 23

Hapa mtoto anaweza kusikia sauti mbalimbali anazozifahamu kama sauti ya mama yake. Mtoto hutumia muda mwingi kulala. Mtoto huwa na uzito wa 660g na urefu wa sentimita 35.

 

Wiki ya 24

Mapafu na mfumo wa upumuaji wa mtoto huendelea kukua. Mapafu ya mtoto hutoa majimaji ambayo husaidia vifuko vidogo vidogo vya hewa kukua. Pia majimaji haya hutunza mapafu ya mtoto yasichubuke na kupata madhara.

 

Wiki ya 25

Wiki hii ni tamati ya theluthi ya pili katika ukuaji wa mtoto. Mfumo wa fahamu wa mtoto huendelea kukua na kuwa imara zaidi, pia ngozi ya mtoto hupata mafuta zaidi ili kuiimarisha na kuifanya iwe laini na nyororo.

 

Wiki ya 26

Mfumo wa fahamu unaweza kuratibisha joto la mwili, pia mafuta mazito meupe huzunguka mfumo wa fahamu ili kuuimarisha zaidi na kuulinda, mtoto anakuwa na uzito wa 1kg.

 

Wiki ya 27

Mtoto anaendelea kukua na mwili wake unatunza akiba ya mafuta. Ubongo wa mtoto hukua kwa kasi katika hatua hii na mtoto huweza kuona na kusikia vizuri kabisa. Viungo vingi vya ndani huwa vimeshakomaa isipokuwa mapafu.

 

Wiki ya 28

Macho ya mtoto yanafunguka vizuri kabisa. Seli nyekundu za damu zinatengenezwa kwenye uroto wa mifupa. Ukuaji wa mtoto katika urefu hupungua na zaidi huongezeka uzito. Mfumo wa upumuaji hukua kwa kasi na mtoto huwa na uzito wa 1.3 kg.

 

Wiki ya 29

Mtoto huendelea kuongezeka uzito. Ngozi yake huzidi kuwa nyororo na sasa huonekana vizuri kama mtoto aliyezaliwa tayari.

 

Wiki ya 30

Vinyweleo vilivyokuwa katika mwili wa mtoto ili kushikilia mafuta yaliyolinda ngozi ya mtoto sasa hutoweka. Kucha za vidole vya mikono zimekamilika na zinaonekana vizuri kabisa.

 

Wiki ya 31

Mtoto huwa na uzito wa 1.9kg kama nanasi na urefu wa zaidi ya sentimita 40. Mapafu na mfumo wa upumuaji unaendelea kuimarishwa. Mifupa huwa migumu bali fuvu hubaki laini bado.

 

Wiki ya 32

Kinga ya mwili ya mtoto hutengenezwa, pia tishu za mafuta huendelea kutengenezwa mwilini kwa mtoto.

 

Wiki ya 33

Mtoto huchukua nafasi ya kutosha katika tumbo la uzazi na maji ya uzazi huendelea kupungua katika plasenta. Mtoto huwa na uzito wa 2.4kg. ngozi inaendelea kuwa nyororo.

 

Wiki ya 34

Kucha za vidole vya miguu huwa zimekuwa vizuri na kuonekana, mtoto anajiandaa kwa ajili ya kutoka tumboni hivyo hulala kichwa kikiangalia chini.

 

Wiki ya 35

Mtoto anakuwa amekamilika kabisa na yuko tayari kutoka nje ya tumbo la mama. Mtoto huendelea na mazoezi ya misuli ya uso kwa kutabasamu.

 

Wiki ya 36

Katika Juma la 36 baada ya kutungwa mimba, mzingo wa kichwa na tumbo la mtoto viko karibu sawa. Mtoto amemwaga lanugo yake yote. Juma hili pia ni wakati wa ukuaji wa lensi.

 

Wiki ya 37

Kifua cha mtoto huonekana vizuri, na via vya uzazi kwa watoto wa kiume hukamilika. Mafuta yanaongezwa mwili mzima wa mtoto ili kumfanya awe na joto baada ya kuzaliwa.

 

Wiki ya 38

Mtoto anakuwa na uzito wa 3.4kg na urefu wa sentimita 50, ukuaji wa mtoto ndani ya tumbo umekamilika hivyo mtoto huwa tayari kuzaliwa.